
Mtoto kucheza tumboni (Quickening)
Hali ya mtoto kucheza tumboni kwa mjamzito (Quickening) ni hali ya mama mjamzito kuanza kuhisi mtoto akicheza tumboni kwa mara ya kwanza kabisa katika kipindi cha ujazito. Huonekana kama miale midogo, mapigo, au mpapaso hafifu. Kwa kawaida hali hii hutokea kati ya wiki ya 16 na 20 ya ujauzito, ingawa baadhi ya wanawake huweza kuhisi mapema au kuchelewa kidogo.
Kuhisi harakati hizi huleta faraja kwa mama kuwa mtoto wake anaendelea kukua vizuri na pia huimarisha uhusiano wa kihisia kati ya mama na mtoto.

Makala zaidi: Kuhusu Ute Mweupe Ukeni: Mambo 5 Usiyoyajua : Sababu, Dalili na Tiba zake.
1.Mtoto kucheza tumboni (Quickening) Utahisi vipi?
Wanawake huelezea kama:
- Kuruka kama kipepeo
- Mipapaso midogo
- Maputo yanavyopasuka
- Mizunguko midogo midogo tumboni au kujiviringisha
- Mishtuko midogo ya misuli tumboni
Mwanzoni hali hii inaweza kuwa ngumu kutambua kama ni mtoto au ni hali ya gesi, lakini kadri wiki zinavyosonga mbele, mama huanza kutambua bayana mtindo wa mtoto na harakati zake huwa wazi zaidi.

2.Mtoto kucheza tumboni (Quickening) huanza lini?
- Mtoto huanza kusogea kuanzia wiki ya 12, lakini mama huwa hajaanza kuhisi chochote hapo mapema.
- Kwa mimba ya kwanza, kawaida huhisiwa karibu wiki ya 18-20.
- Kwa waliowahi kupata mimba, harakati huweza kuhisiwa mapema zaidi, takribani wiki ya 16-18.
Baadhi ya Mambo yanaweza kuyoathiri muda wa kuhisi mtoto kucheza tumboni (quickening):
- Ikiwa ni mimba ya kwanza au sio.
- Mahali kondo la nyuma lilipo jishikiza (placenta attachment).
- Asili ya Hurka ya mtoto (anaweza kuwa mtulivu au mchangamfu zaidi).
3.Utahisi harakati Upande gani wa tumbo?
Kwa kawaida utahisiwa chini ya kitovu, karibu na mfupa wa yonga au karibu na kinena. Kadri mimba inavyokua na mfuko wa uzazi huwa unapanda juu zaidi, hivyo harakati za mtoto kucheza utazihisi sehemu za juu zaidi.

Makala zaidi: Dawa ya uvimbe kwenye kizazi Bila Upasuaji
4.Ni mara ngapi unatakiwa kuhisi?
Kufikia wiki ya 20–24, mama hutakiwa kuhisi mtoto akicheza mara kwa mara. Kufikia kipindi cha tatu cha ujauzito (takriban wiki ya 28), mama anatakiwa kuhisi angalau michezo 10 ndani ya masaa 2.
Ukihisi harakati chache, usiwe na hofu mara moja—lakini mjulishe daktari au mkunga kwa uhakika- kama mtoto wako hajacheza siku nzima.

5.Kucheza kucheza (Quickening) hubadilika kuwa mateke/kicks lini?
Kufikia kipindi cha tatu cha ujauzito (Third trimester), mtoto huanza kupiga miguu kwa nguvu zaidi, kupiga ngumi, kujiviringisha, na hata kucheua (hiccups).
Mama huanza kuona mpangilio na mkao maalum wa mtoto wake. Kupiga hesabu za miguu husaidia kutambua hali ya kawaida na kubaini mabadiliko.
6.Kwa nini mtoto hujongea tumboni?
kujongea na kucheza husaidia ukuaji wa mifupa, misuli na viungo vya mtoto. Pia humwandaa mtoto kwa maisha ya baadae nje ya tumbo. Kukosa harakati na kujongea kabisa kunaweza kuashiria tatizo kwenye kondo la nyuma au kwenye maji ya uzazi, hivyo ni vyema kumjulisha daktari endapo una wasiwasi mwanao hachezi.
7.Je, mtoto kucheza (quickening) kunaweza kutoweka kisha kurudi?
Ndiyo. Watoto huwa na nyakati za kulala na kuamka. Hivyo ni kawaida kuhisi harakati na mijongeo kisha zikakoma kwa muda fulani halafu baadae zikarudi. Kadri zinavyokuwa na nguvu, huwa za kawaida na thabiti zaidi.
8.Njia za kumchochea mtoto Kucheza:
- Kunywa kitu chenye utamu kama matunda au juisi.
- Kula chakula kizuri unachokipenda.
- Fanya zoezi la Kutembea kidogo.
- Baba wa mtoto kushika au kupapasa tumbo.
- Kusikiliza muziki mzuri au mama kuzungumza na mtoto mwenyewe.
- Kukaa kimya na kutuliza mawazo.

9.Wakati Gani wa kumpigia daktari:
- Kama baada ya wiki ya 28 hujahisi harakati na mijongeo angalau 10 ndani ya masaa 2.
- Ikiwa harakati na mijongeo ghafla zimepungua au kusimama kwa siku kadhaa.
10. Je, Mtoto kucheza (quickening) inaleta maumivu?
Hapana. Harakati za mtoto hazipaswi kuleta maumivu. Ikiwa unapata maumivu au mikakamao mikali, mjulishe daktari au mkunga wako ili akusaidie kubaini tatizo.
Hitimisho
Kuhisi harakati za kwanza za mtoto tumboni ni hatua ya kusisimua zaidi kwa mama. Kwa kawaida hutokea karibu wiki ya 16-20, lakini kila mimba ni tofauti. Ikiwa una wasiwasi kuhusu harakati na mijongeo ya mtoto wako, wasiliana na mtoa huduma wako wa afya ili upate uhakika.







