Saratani ya Utumbo Mpana (Colon Cancer)
Saratani ya utumbo mpana ni aina ya saratani inayotokea pale vinundu vidogo vinavyoitwa polyps vinapoota kwenye ukuta wa ndani wa utumbo mpana au sehemu ya mwisho ya utumbo (rectum). Mara nyingi huanza kama uvimbe usio na madhara, lakini unaweza kubadilika na kuwa saratani kadiri miaka inavyopita.
Kupima mapema (screening) na kuondoa polyps kabla havajageuka saratani hupunguza kwa kiwango kikubwa hatari ya ugonjwa huu.
Dalili za Saratani ya Utumbo Mpana
Saratani hii ya utumbo mpana yenyewe hukua pole pole na huchukua muda ili kuweza kuonekana.
Dalili zinapoanza kujitokeza, zinaweza kujumuisha:
Maumivu ya tumbo yasiyoisha
Tumbo kujaa au kuvimba
Damu kwenye kinyesi
Kuharisha au kufunga choo mara kwa mara
Hisia ya kutomaliza haja kubwa kabisa
Uchovu usio na sababu
Kupungua uzito bila sababu
Dalili hizi zinaweza pia kusababishwa na magonjwa mengine, lakini ukizipata kwa zaidi ya siku kadhaa ni muhimu kumuona daktari.
Sababu na Vihatarishi
Saratani ya utumbo hutokea pale seli za utumbo zinapobadilika kitabia (genetic mutations) na kuanza kukua bila mpangilio. Hatari huongezeka kwa:
Umri wa zaidi ya miaka 50 (lakini inaongezeka hata kwa walio chini ya miaka 50)
Historia ya familia yenye saratani ya utumbo au polyps
Kuwa na polyps nyingi
Magonjwa ya kurithi kama Lynch syndrome
Uzito uliopitiliza (BMI>25)
Uvutaji sigara
Ulevi (hata kiasi cha wastani kinaongeza hatari)
Jinsi Saratani ya Utumbo Inavyogunduliwa
Daktari anaweza kutumia vipimo mbalimbali:
Vipimo vya damu kama CBC, CMP, CEA
Vipimo vya picha kama CT scan, MRI, PET scan, Ultrasound
Colonoscopy hiki ni kipimo muhimu zaidi; kinaweza kuona polyps na kuondoa kipande cha tishu kwa uchunguzi
Majibu ya vipimo hutumika pia kubaini hatua ya saratani (cancer staging), ambayo huamua namna ya matibabu.
Hatua za Saratani ya Utumbo Mpana
Hatua 0:Seli zisizo za kawaida lakini bado hazijawa saratani kamili (zipo kwenye polyp).
Hatua I: Saratani imeingia kwenye ukuta wa utumbo lakini haijasambaa.
Hatua II: Saratani imepenya zaidi kwenye ukuta wa utumbo.
Hatua III:Saratani imeenea kwenye tezi za limfu karibu na utumbo.
Hatua IV: Saratani imesambaa kwenye viungo vya mbali kama ini, mapafu au ovari.
Matibabu kwa mgonjwa wa saratani ya utumbo mpana:
Matibabu hutegemea hatua ya saratani:
Upasuaji
Polypectomy: Kuondoa polyps wakati wa colonoscopy
Colectomy:Kuondoa sehemu ya utumbo iliyoathirika.
Chemotherapy
Mionzi (Radiation therapy)
Targeted therapy hizi ni dawa maalum zinazolenga Selimadhara za saratani
Kwa hatua za mapema, upasuaji pekee unaweza kuponya kabisa.
Wakati wa Kumwona Daktari
Mwone daktari mara moja ukiwa na:
Damu kwenye kinyesi
Maumivu ya tumbo yasiyoisha
Kupungua uzito bila sababu
Kuharisha au kufunga choo kwa muda mrefu
Utabiri na Uhai (Prognosis)
Kiwango cha kuishi miaka 5 kulingana na sehemu saratani ilipofika:
Localized (bado haijasambaa): 91%
Regional (imetoka nje ya utumbo kwenda maeneo jirani): 73%
Distant (imesambaa mbali): 13%
Hii ni takwimu za watu wengine kila mgonjwa ana safari yake kulingana na hatua, afya ya jumla, na aina ya matibabu.
Jinsi ya kujikinga na saratani ya utumbo mpana.
Huwezi kuzuia saratani kikamilifu, lakini unaweza kupunguza hatari kwa:
Kula lishe yenye mboga, matunda, nafaka zisizokobolewa, na protini isiyo na mafuta mengi
Kuacha kuvuta sigara
Kupunguza au kuacha pombe
Kuweka uzito sahihi
Kufanya screening kuanzia miaka 45 au mapema zaidi kama una historia ya familia
Hitimisho
Saratani ya utumbo mpana hukua taratibu na mara nyingi haina dalili za mapema. Uchunguzi wa mara kwa mara ni njia bora ya kuzuia ugonjwa huu au kuugundua mapema kabla haujasambaa. Ikiwa utagunduliwa, usikate tamaa matibabu ya hatua za awali yana kiwango cha juu sana cha kupona.
Maswali Yanayoulizwa Mara Kwa Mara (FAQs) Kuhusu Saratani ya Utumbo Mpana
- Je, saratani ya utumbo mpana ina dalili za mapema?
Kwa kawaida hapana. Saratani hii ina desturi au tabia ya kukua taratibu mno huku ikichukua miaka mingi na bila kuonyesha dalili yoyote ile. Ndiyo maana screening ni muhimu. Dalili hujitokeza tu ikiwa saratani imeanza kukua na kuathiri tishu au kusambaa. - Ni dalili zipi ninazopaswa kuziangalia kwa makini?
Dalili muhimu ni pamoja na:
Damu kwenye kinyesi
Maumivu ya tumbo yasiyoisha
Kubadilika kwa mfumo wa choo (kuharisha au kufunga)
Kupungua uzito bila sababu
Uchovu mwingi
Ukiona dalili hizi kwa zaidi ya siku chache, muone daktari. - Polyps ni nini?
Polyps ni vijivimbe vidogo vinavyoota kwenye ukuta wa ndani wa utumbo. Si vyote ni saratani, lakini vingine vinaweza kubadilika na kuwa saratani kadiri muda unavyopita. - Je, polyps zikitolewa zinazuia saratani?
Ndiyo. Kuondoa polyps mapema kupitia colonoscopy hupunguza hatari ya kupata saratani ya utumbo kwa kiwango kikubwa sana. - Je, saratani ya utumbo hurithiwa?
Watu wenye historia ya familia ya saratani ya utumbo au polyps wana hatari kubwa zaidi. Pia magonjwa ya kurithi kama Lynch syndrome yanaongeza hatari. - Je, watu walio chini ya miaka 50 wanaweza kupata saratani ya utumbo?
Ndiyo. Idadi ya vijana chini ya miaka 50 wanaopata saratani hii imeongezeka katika miaka ya karibuni, ingawa hakuna sababu moja ya moja iliyothibitishwa. - Screening ya saratani ya utumbo inaanza lini?
Kwa kawaida inapendekezwa kuanza miaka 45, lakini kama una historia ya familia au hatari kubwa, unaweza kuanza mapema zaidi (muone daktari kwa ushauri). - Vipimo gani hutumika kugundua saratani ya utumbo mpana?
Vipimo vikuu ni:
Colonoscopy
CT scan, MRI, PET scan
Vipimo vya damu (CEA, CBC)
Ultrasound
Colonoscopy ndiyo kipimo cha msingi na cha uhakika zaidi. - Je, saratani ya utumbo inatibika?
Ndiyo, hasa ikigunduliwa mapema. Saratani ya hatua ya awali mara nyingi hutibika kabisa kupitia upasuaji na, ikihitajika, chemotherapy au mionzi. - Matibabu yake ni ya muda gani?
Inategemea hatua ya saratani.
Hatua za awali: upasuaji pekee, kupona haraka.
Hatua za kati: upasuaji pamoja na chemotherapy.
Hatua za juu: matibabu ya muda mrefu zaidi (chemotherapy, targeted therapy, mionzi). - Je, maisha yangu yatakuwa vipi baada ya matibabu?
Wagonjwa wengi huishi maisha ya kawaida baada ya matibabu, hasa wale waliogunduliwa mapema. Ufuatiliaji wa mara kwa mara unahitajika ili kuona kama saratani imerudi. - Naweza kufanya nini kupunguza hatari ya kupata saratani ya utumbo?
Kula lishe yenye mboga, matunda na nafaka zisizokobolewa
Kuacha sigara
Kuepuka pombe
Kufanya mazoezi
Kuweka uzito sahihi
Kufanya screening mara kwa mara - Je, saratani ya utumbo inaweza kurudi baada ya matibabu?
Inaweza kurudi, hasa kama iligunduliwa katika hatua ya juu. Ndiyo maana ufuatiliaji wa kitabibu ni muhimu kwa miaka kadhaa baada ya matibabu. - Je, damu kwenye kinyesi ni lazima iwe saratani?
Si lazima. Inaweza kutokana na bawasiri, vidonda, maambukizi au sababu nyingine. Hata hivyo, damu kwenye kinyesi ni dalili muhimu muone daktari kila mara inapojitokeza. - Mtu anaweza kuishi kwa muda gani baada ya kugunduliwa na saratani ya utumbo?
Hili hutegemea hatua ya saratani, umri, afya ya mgonjwa na aina ya matibabu. Katika hatua za awali, kiwango cha kupona ni juu sana. Katika hatua za juu, matibabu hulenga kupunguza dalili na kuongeza muda wa kuishi.